Kujiua ni moja ya matatizo yanayoongezeka kwa nchini Tanzania na duniani. Watu wengi wanapitia maumivu makubwa kimya kimya huku wakikosa mtu wa kuwasikiliza na kuwasaidia.
Watu wanaofikiria kujiua hawataki kufa; wanataka tu kukomesha maumivu yao yasiyovumilika. Kwao, kifo kinaonekana kama “dawa” pekee ya kuzima maumivu hayo. Wanaamini kua hakuna njia nyingine ya kupata nafuu.
Katika makala hii utajifunza:
- Sababu kuu zinazowafanya watu wafikirie kujiua
- Dalili za mtu anayepitia msongo mkubwa wa mawazo
- Suluhisho la kisaikolojia
- Suluhisho la Kibiblia
- Hatua za kuchukua kama unahisi umefika mwisho
Kwa Nini Watu Wanajiua?

1. Kupoteza Tumaini la Maisha
Mtu anapoona maisha hayabadiliki, anaweza kuanza kuhisi hakuna sababu ya kuendelea kuishi.
Wengine hupitia:
- Hali ya umaskini mkubwa
- Kuvunjika kwa mahusiano au ndoa
- Kukosa kazi kwa muda mrefu
- Kushindwa kutimiza ndoto na malengo yao
- Magonjwa ya muda mrefu
Mfano wa Biblia
Yuda Iscariote alikata tamaa baada ya kuona makosa yake hayawezi kusamehewa. Akaamua kujinyonga mwenyewe.

2. Msongo wa Mawazo na Upweke
Watu wengi wanaopitia depression hujifungia ndani na kuamini hakuna anayewaelewa.
Upweke wa muda mrefu unaweza kufanya mtu ahisi:
- Hana thamani
- Hasikilizwi
- Ameachwa peke yake duniani
Mfano wa Biblia
Nabii Eliya aliwahi kufika hatua ya kuomba afe kutokana na uchovu wa kihisia.

3. Hatia na Aibu ya Makosa ya Zamani
Baadhi ya watu wanabeba majeraha ya zamani kwa miaka mingi.
Makosa yaliyopita yanaweza kumfanya mtu aamini:
- Hastahili kusamehewa
- Hana Thamani tena
- Maisha yake yameharibika milele
Lakini ukweli ni kwamba Mungu bado anaweza kurejesha maisha yoyote.
Mfano wa Biblia
Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji.

Dalili za Mtu Anayefikiria Kujiua
Ukiona dalili hizi kwako au kwa mtu mwingine usizipuuze.
- Kujitenga: Anajiondoa kwenye vikundi vya marafiki na familia.
- Maneno ya Kukata Tamaa: Anazungumza kuhusu kuhisi amekwama au kuwa mzigo kwa wengine.
- Mabadiliko ya Kihisia: Analia mara kwa mara au ana huzuni nzito ya kudumu.
- Matatizo ya Usingizi: Anakosa usingizi kabisa au analala kupita kiasi.
- Kupoteza Nia: Haonyeshi tena hamu na mambo aliyokuwa akiyapenda awali.
- Kugawa Mali: Anaanza kutoa vitu vyake vya thamani kwa watu wengine kama zawadi ya mwisho.
- Mabadiliko ya Ghafla: Anaonekana kuwa na utulivu wa ajabu baada ya kipindi kirefu cha huzuni (hii inaweza kuwa ishara kuwa ameshafanya maamuzi).
Suluhisho la Kisaikolojia kwa Mtu Anayefikiria Kujiua

1. Zungumza na Mtu Unayemwamini
Usikabiliane na maumivu ya moyo peke yako. Kushirikisha wengine hupunguza uzito wa matatizo unayopitia.
Watu unaoweza kuzungumza nao:
- Watu wa Karibu: Rafiki, mzazi, au mlezi.
- Wenza: Mume, mke, au mpenzi.
- Viongozi wa Kiroho: Mchungaji, Imamu, au kiongozi wa dini.
- Wataalamu: Washauri wa saikolojia na madaktari wa afya ya akili.

2. Tafuta Msaada wa Kitaalamu
Afya ya akili ina thamani sawa na afya ya mwili. Kutafuta msaada wa kitabibu si udhaifu, bali ni hatua ya hekima na ujasiri. Biblia inatukumbusha kuwa “Pasipo mashauri makusudi hubatilika.” (Mithali 15:22).
Nchini Tanzania kuna wataalamu wa afya ya akili wanaoweza kusaidia kuratibu mawazo na hisia zako kwa usahihi.

3. Mawazo Yako Si Ukweli Kila Wakati
Akili inaweza kukudanganya nyakati za maumivu. Mawazo hasi mara nyingi ni zao la hisia kali, si ukweli wa mambo. Kumbuka, hali unayopitia sasa ni ya mpito na inaweza kubadilika kuwa bora.
Mifano ya kauli potofu za akili:
- “Hakuna mtu anayenipenda au kunijali.”
- “Hakuna tumaini lolote lililobaki.”
- “Maisha yangu hayawezi kubadilika tena.”

Suluhisho la Kibiblia kwa Mtu Aliyekata Tamaa

1. Mungu Anaona Thamani Yako
Uwepo wako duniani si ajali; uliumbwa kwa kusudi maalum. Hata kama umechoka au unahisi umekataliwa na watu, thamani yako mbele za Mungu haijapungua. Yeye anakujua kwa jina na ana mpango na maisha yako.

2. Mungu Ana Mpango Mwema na Wewe
Maandiko ya Yeremia 29:11 yanatukumbusha kuwa Mungu ana mawazo ya amani na tumaini juu ya maisha yako. Hata kama leo unaona giza nene, kesho yako bado ina nafasi ya kubadilika na kuwa angavu. Maumivu ya sasa si mwisho wa hadithi yako.

3. Yesu Anakualika Upumzike Kwake
Kama umechoka na kuelemewa na mizigo, Yesu anakupa mwaliko wa kupumzika. Mathayo 11:28 inasema, “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Huna sababu ya kupigana na maumivu yako peke yako. Yuko tayari kubeba mzigo wako.

Hatua za Dharura: Nifanye Nini Nikihisi Nataka Kujiua Leo?
Ikiwa unahisi kutaka kukatisha maisha yako leo, simama kwanza. Maumivu unayosikia ni makali, lakini ni ya muda. Usifanye uamuzi wowote wa kudumu leo.
1. Usalama wa Kimwili (Nini Usifanye)
- Ahirisha Uamuzi: Usifanye maamuzi yoyote ya haraka leo. Subiri kwanza; hisia kali hupanda na kushuka.
- Usikae Peke Yako: Toka chumbani au eneo lililojitenga. Nenda mahali penye watu au nje kwenye mwanga.
2. Msaada wa Kijamii (Nini Ufanye Nje)
- Tafuta Mtu: Piga simu au nenda kwa mtu unayemwamini mara moja. Mweleze unachohisi.
3. Msaada wa Kiroho (Nini Ufanye Ndani)
- Omba kwa Uwazi: Mwambie Mungu ukweli wote kuhusu maumivu na uchovu wako.
- Soma Neno: Tafuta faraja kupitia Zaburi ya 23, Zaburi ya 34, au Zaburi ya 91.
Hitimisho: Chagua Maisha, Kuna Tumaini Jipya Leo
Maumivu ya kisaikolojia yanaweza kuficha mwanga wa matumaini. Lakini kumbuka: kujiua ni suluhisho la kudumu kwa tatizo la muda mfupi. Hali unayopitia sasa haina mamlaka ya kuamua mwisho wa maisha yako. Mungu anakupenda, na Tanzania inahitaji mchango wako.

